KUONDOLEWA kwa Nape Nnauye katika wadhifa wa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, kisha saa chache baadaye kutishiwa bastola
wakati akielekea kuzungumza na waandishi wa habari, kumejenga taswira
pana.
Taarifa kutoka ndani ya mifumo ya Serikali zinaeleza kuwa awali Nape
alisikika akilalamika kwa watu wake wa karibu, kwamba anajua Rais Dk.
John Magufuli ana mpango wa kumwondoa kwenye baraza lake la mawaziri.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, malalamiko yake hayo yalianza kusikika hata
kabla ya sarakasi za kiongozi mmoja wa Serikali kuvamia kituo cha
televisheni na redio cha Clouds.
Watu wa karibu na Nape wanasema kuwa alipata kufikisha malalamiko yake
hayo kwa baadhi ya viongozi wastaafu ambao wamepata kutumikia nyadhifa
za juu serikalini.
Ingawa hakuna chombo chochote kilichokuwa tayari kuthibitisha hilo,
lakini zipo taarifa zinazodai kuwa mwelekeo wa Nape kutenguliwa uwaziri
ulitokana na mwanasiasa huyo kupishana misimamo na uongozi wake wa juu.
Taarifa kwamba Nape aliliona anguko lake, zinathibitishwa na maandiko yake mwenyewe kupitia akaunti yake ya twitter.
Andiko lake la hivi karibuni ni lile la Machi 20, mwaka huu ambalo linasomeka; “No longer at Ease!” (hakuna lisilo na mwisho).
Siku hiyo hiyo aliandika tena; “Each day is a day of decision and our
decisions determine our desitiny!” (kila siku ni siku ya uamuzi, na
maamuzi yetu huamua mwisho wetu)
Akandika tena “Mungu mkubwa!“ Na siku hiyo hiyo alituma ujumbe
unaosemeka; “Majaribu huja ili kutuinua kutoka utukufu hadi utukufu.
Kikubwa tusikate tamaa! Utukufu mkubwa upo mbele! Kwaresma njema.”
Machi 18, mwaka huu aliandika; “Chura akipigwa teke…” na Machi 14 akaandika “Brand hulindwa!”
Machi 9 aliandika; “Criticism may not be agreable but its necessary. It
fulfils same function as pain in the body. It calls atention to an
unhealthy state of things (ukosoaji unaweza usikubalike lakini ni
muhimu. Unafanya kazi sawa na maumivu mwilini. Inakidhi kazi ile ile ya
maumivu ya mwili. Ni wito wa tahafari kwa hali mbaya ya mambo)
Ni nyakati kama hizo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimfutilia Nape,
wanasema ndipo alipoonekana hadharani kuikosoa Serikali tofauti na siku
za nyuma.
Mfano mmojawapo ni wakati wa sakata la dawa za kulevya alipoonekana wazi
kumkosoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliyeibuka hivi karibuni na
orodha ya watuhumiwa wa dawa za kulevya, wakiwamo wasanii.
Nape alishauri hatua zinazochukuliwa ziepuke kuharibu nembo ya biashara
aliyojijengea msanii husika kwa sababu ni gharama kubwa kuirejesha.
Siku chache baadae, Rais Magufuli alisikika akisema vita ya dawa za
kulevya haina umaarufu. Pasipo kutaja jina, alieleza kushangazwa na wale
waliokuwa wakiwatetea watuhumiwa.
Ni tangu wakati huo inaelezwa kuwa Nape amekuwa akiandika ujumbe mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii na hivyo kuzua gumzo.
Ukiachilia mbali kuandika ujumbe kwenye akaunti yake ya twitter, pia
Nape alionekana kutoa kauli nzito zenye kuashiria kukata tamaa
kuitumikia nafasi hiyo.
KUVAMIWA CLOUDS
Tofauti na misimamo ya Nape katika siku za nyuma ambayo ilijiegemeza
zaidi kuitetea Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika tukio la
uvamizi wa kituo cha Clouds, alionyesha taswira nyingine kwa kukemea
kitendo hicho na hata kuchukua hatua ya kuunda kamati kuchunguza.
Wakati Nape akichukua hatua hiyo, baadae siku hiyo hiyo Rais Magufuli
alisikika akimtaka kiongozi anayetuhumiwa kufanya uvamizi huo achape
kazi.
Siku moja baada ya Nape kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza
tukio hilo na kutanabaisha wazi kwamba anajua kutetea haki kuna gharama
zake, hivyo yuko tayari kuzilipa, Rais Magufuli alitangaza kumwondoa
katika nafasi yake ya uwaziri.
Watu wanaomfahamu Nape na ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa ukaribu,
wameliambia MTANZANIA Jumapili kuwa mwanasiasa huyo alijua wazi anguko
lake.
“Hebu nyinyi waandishi wa habari jiulizeni ni lini Nape alikuwa rafiki
wa vyombo vya habari kama si sasa? Ni kwa sababu alijua. Huko nyuma
hakuwa upande wenu, mnakumbuka kuhusu sheria ya huduma ya vyombo vya
habari?” alihoji mbunge mmoja wa CCM ambaye hakutaka jina lake liandikwe
gazetini.
MUSWADA WA SHERIA YA HABARI
Nape alijipambanua vizuri kutetea msimamo wa Serikali wakati wa mchakato
wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari ambao
ulipitishwa na Bunge wakati kukiwa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau
wa habari.
Katika jitihada za kupitisha muswada huo, Nape alisimama kidete
kuhakikisha mjadala wa kuupitisha hausogezwi mbele kama ilivyoombwa na
wadau wa habari ambao walitaka kupata muda wa kuusoma ili waongeze maoni
yao na kukosoa vipengele ambavyo vinaonekana ni kandamizi kwa tasnia.
Mwanzo wa uongozi katika wizara hiyo, Nape alinyooshewa kidole na
wafuatiliaji wa mambo kuwa yeye ndiye aliyeongoza jitihada za Serikali
za kuzuia televisheni nchini zisionyeshe vikao vya Bunge la 11
mubashara.
Wakati wa mjadala wa sakata hilo bungeni, Nape alitetea msimamo huo wa
kulizuia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwamba lisionyeshe Bunge
mubashara kwa kigezo cha kushindwa kuhimili gharama.
Katika ufafanuzi wake juu ya sakata hilo, Nape alisema msimamo wa
kuifungia TBC isionyeshe Bunge mubashara umetolewa na Serikali, lakini
akasema hajavizuia vyombo binafsi.
Kupitia maelezo hayo, alijitetea kwamba uamuzi wa kuzuia matangazo hayo
ulifanywa na Bunge la Kumi wakati likipitisha uamuzi wa chombo hicho wa
kuanzisha studio yake.
Siku chache baadaye, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa nchini Uingereza,
alikazia hoja hiyo kwa kusema sababu ya kuzuia matangazo mubashara ya
Bunge ni kutoa nafasi kwa wananchi kufanya kazi kwani walikuwa hawafanyi
kazi.
Hata hivyo, tukio la sasa la Nape kupinga utendaji kazi wa Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam limeonekana kufuta matukio yake ya nyuma ambayo baadhi
ya watu, hasa upande wa upinzani, walikuwa wakiyachukulia kwa mtazamo
hasi.
MKUTANO WAKE ULIVYOZUA HOFU
Upo mtazamo kuwa pengine kubadilika huko ghafla misimamo ya Nape
kulichangia kwa kiasi kikubwa kuzuiwa kwa mkutano wake na waandishi wa
habari saa chache baada ya Rais Magufuli kumwondoa katika wadhifa wake.
Hata hivyo, taarifa za kuzuiwa kwa mkutano huo hadi sasa ni za
kukanganya, hasa baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Susan
Kaganda kukanusha taarifa za Meneja wa Hoteli ya Protea
aliyejitambulisha kwa jina moja la Suleiman kwamba alipata maelekezo
kutoka kwake ya kutoruhusu kufanyika hotelini kwake.
Pamoja na hilo, tukio la kujitokeza mtu aliyetoa bastola hadharani
kumtishia Nape ili arudi ndani ya gari, nalo lilijenga taswira hiyo
hiyo.
CREDIT - MTANZANIA
Post a Comment