CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema nyumba iliyopo Mtaa
wa Ufipa katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, inamilikiwa
na chama hicho kupitia Baraza la Wadhamini.
Chadema imetoa ufafanuzi kutokana na taarifa zilizosambaa katika
mitandao ya kijamii kuwa wamepewa notisi ya siku 14 na mmiliki wa jengo
hilo, wanalotumia kama ofisi na Makao Makuu ya chama hicho, kuhama
kutokana na kukiuka mkataba wa malipo na upangishwaji.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akijibu uvumi huo, alisema chama
hicho ni mmiliki halali wa jengo la Makao Makuu lililo chini ya Baraza
la Wadhamini.
“Kama kuna mmiliki wa jengo hilo ajitokeze, lakini nawahakikishia hakuna
hivyo puuzeni habari zinazozagaa,” alisema Makene na kuongeza kuwa kuna
hati ya jengo hilo, iliyoandikwa mmiliki wa jengo hilo ni Chadema.
Alisisitiza watu wapuuzie propaganda hizo, zinazopanga kuwahadaa
wanachama na Watanzania kwa ujumla.
Post a Comment