Nakiri kuwepo kwa mgogoro wa kibiashara wa miaka mingi baina ya Kampuni hii na NHC. Aidha kampuni hii imekuwa ikilipa kodi stahiki kwa NHC kwa mujibu wa makubaliano yetu ya kibiashara.
Kumekuwepo na ukakasi wa muda mrefu kuhusiana na mkataba wetu wa umiliki, uendelezaji na uendeshaji wa jengo hili unaochagizwa na msimamo wangu wa kisiasa.
Haki na Uhuru wetu wa kufanya biashara kama raia wengine umekuwa ukiingiliwa mara kwa mara katika mazingira yanayoambatana na Vitisho kiasi ambacho Maamuzi kadhaa hayafanyiki kwa hofu ya kisiasa kwamba “Itakuwa kumwongezea nguvu Mpinzani”. Hivyo, ningependa umma wa Watanzania uelewe kuwa sidaiwi na Shirika la Nyumba la Taifa(NHC). Kufuatia utata huu wanasheria wa Kampuni wanashughulikia jambo hili kwa taratibu za kibiashara na kisheria.
Naomba kuweka wazi kwa yeyote anayehusika. Sitafungwa fikra, sitafungwa mdomo na sitaacha kuutetea Ukweli, Haki na Demokrasia katika nchi hii kwa misingi ya “kulinda kinachodhaniwa ni maslahi yangu ya kibiashara”. Wafanyabiashara wengi wanafungwa fikra na midomo ndani ya nchi hii kwa kuogopa hila na ghiliba za watawala.
Ni heri kufa masikini nikiwa nimesimamia ukweli, kuliko kuishi tajiri niliyetawaliwa na ubinafsi, woga, hofu na ubatili.
Natambua kuna jitihada za kutumia kila silaha na kila hila dhidi yetu katika Kipindi hiki.
Mwisho, Natoa rai kwa wanachama na wapenzi wa Haki katika Taifa hili, wasiogope. Haki itaweza kucheleweshwa kwa muda tu, lakini kamwe haiwezi kuzuiwa. Binadamu akikufungia mlango Mungu wa Haki atakufungulia dirisha.
Ubatili ni wa mpito lakini Haki ni ya milele.
Post a Comment