Ni asubuhi tulivu katika fukwe za bahari ya hindi kusini mwa Tanzania ambapo vijana wengi wamejitokeza kufanya usaili wa mashindano ya Maisha Plus East Africa 2016. Wapo wanaoonekana kujiamini na wengine wamejawa uoga. "Ni siku niliyoisubiri kwa hamu sana" anasema Faustine Komba miongoni mwa washiriki kutoka Mtwara.
Safari ya msimu wa tano wa mashindano ya Maisha Plus imeanza rasmi kwa kuanza na usaili uliofanyika katika hotel ya NAF Beach iliyoko Mtwara. Washiriki kutoka mikoa ya jirani nao pia walijitokeza. "Maisha Plus kwangu ni ndoto ya muda mrefu sana, niliposikia mnakuja Mtwara nikasema piga ua lazima nishiriki" Anasema Ismail Likando aliyesafiri kutoka Lindi.
Maswali mengi yalilenga kupima uelewa wa vijana kuhusu mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo mtazamo wao juu ya mwenendo wa kiuchumi. Mengine yalilenga kuwachanganya tu.
Mshiriki Grace Pemba anaelezea changamoto mbalimbali alizokutana nazo kutokana na kuolewa akiwa na umri mdogo, anasema hadi sasa ana watoto wawili ambao wanaishi na baba yao. Alipoulizwa maswali zaidi Grace alijawa na simanzi na kujikuta akitoa machozi, "Nimelia kwa sababu mmenikumbusha nyuma nilikotokea" anasema Grace mfanyakazi wa Saloon kutoka mkoani Mtwara.
A video posted by Maisha Plus (@maishaplus2016) on Jun 4, 2016 at 6:47am PDT
Wakati usaili ukiendelea hali ya kujaa kwa maji baharini ilitokea na kulazimisha timu ya Maisha Plus kubadili utaratibu wa awali wa upigaji picha.
- Waandaaji wa mashindano ya Maisha Plus wakibadili utaratibu wa awali wa kupiga picha baada ya maji kujaa.
Muhitimu wa shahada ya kilimo William Mbaga alibanwa kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali ikiwemo faida za kilimo cha 'greenhouse' pamoja na namna ambavyo maziwa ya mtindi yanapatikana. William alijieleza kwa ujasiri.
Washiriki wenye fani na ujuzi mbalimbali walijitokeza wakiwemo madereva bodaboda, mafundi, waigizaji, waimbaji, wasusi n.k
- Waigizaji pia walikuwemo katika usaili wa #MaishaPlusMtwara
- Washiriki mbalimbali waliojitokeza katika usaili wa #MaishaPlusMtwara.
Mashindano ya Maisha Plus kwa mwaka huu yanatarajia kuchukua washiriki 30 kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Kenya, Tanzania na Uganda ambapo mshindi atajishindia ufadhili wa wazo la biashara lenye thamani ya Tzshs. Milioni 30.
"Mwaka huu washiriki wajipange sana. Maandalizi yaliyofanywa kufanikisha msimu huu hayajawahi kutokea katika historia ya Maisha Plus. Ni kama tunaanza moja" Alisema Masoud Kipanya, miongoni mwa majaji na waanzilishi wa mashindano haya.
"Tumewekeza katika teknolojia ya kisasa ili kupata picha za matukio yenye uhalisia zaidi. Watazamaji wategemee burudani safi isiyomithirika kupitia Azam Two." Alisema David Sevuri, miongoni mwa waanzilishi wa Maisha Plus.
Taarifa mbalimbali kuhusu mashindano haya zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya www.maishaplus.tv
Post a Comment