Mgeni
Rasmi Afisa Elimu Manispaa ya Moshi, Bw. Deo Tulo Fundi (pichani kulia)
akifafanua jambo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kompyuta zenye matini
ya masomo tisa ya Sekondari (kidato cha kwanza – sita), kompyuta hizo
zilitolewa na Shule Direct kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wenye ulemavu
wa kusikia katika Shule ya Ufundi Sekondari Moshi. (Kushoto ni Bw.
Erasmus Kyara, Mkuu wa Shule ya Ufundi Moshi).
Afisa
Elimu wa Elimu ya Mahitaji Maalum Manispaa ya Moshi akitoa neno wakati
akishuhudia tukio la makabidhiano ya kompyuta zenye matini za kujifunzia
zilizotolewa na Shule Direct kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa
kusikia katika Shule ya Ufundi Sekondari Moshi.
Baadhi
ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia katika Shule ya Ufundi Sekondari
Moshi na mwalimu wao Mwl. Raphael Lukumai (aliyekaa kulia) wakifurahia
pamoja na baadhi ua wageni waliofika shuleni kwao kukabidhi kompyuta
zenye masomo tisa ya Sekondari ndani yake.
Baadhi
ya wanafunzi wa shule ya ufundi sekondari Moshi wakielekezana jambo
katika mojawapo ya kompyuta walizokabidhiwa na Shule Direct, shuleni
kwao,
Aneth
Gerana, mtanzania wa kwanza mwenye ulemavu wa kusikia kupata shahada ya
Chuo Kikuu, ambaye pia alijitokeza kuunga mkono jitihada za Shule
Direct, akiongea na baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia katika
shule ya ufundi sekondari Moshi wakati wa hafla fupi ya kukabidhi
kompyuta shuleni hapo.
Aneth
Gerana na baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia kutoka shule ya
ufundi sekondari Moshi, wakifurahia kompyuta zilizotolewa na Shule
Direct ili kuwasaidia wanafunzi hao kujifunza kwa urahisi zaidi.
Faraja
Nyalandu, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa Shule Direct na Aneth
Gerana wakikimbia mbio za kilometa 21.1 wakati wa mbio za Kili Marathon.
Shule Direct walishiriki mbio hizo kwa ajili ya kuchangisha fedha
kuwezesha upatikanaji wa kompyuta zenye matini ya masomo tisa ya
Sekondari kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia
katika shule za Ufundi Sekondari Moshi na Njombe Sekondari ya viziwi.
Wakiwa
wenye nyuso za furaha, Faraja Nyalandu, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu
wa Shule Direct, Aneth Gerana na wengine kutoka Shule Direct na marafiki
wa Shule Direct mara baada ya kumalizi mbio za kilometa 21.1 wakati wa
Kili Marathon.
Namna
bora ya kufundisha wanafunzi wenye ulemavu ni kuwafundisha wakiwa
wamechanganyika darasa moja na wanafunzi wasio na ulemavu. Hii
inamaanisha kwamba kwa wanafunzi wasiosikia ni muhimu walimu
watakaofundisha hilo darasa wawe ni wataalamu wa lugha ya ishara ili
waweze kufundisha kwa matamshi na ishara ili kukidhi mahitaji ya wote.
Hii ni ngumu kwasababu si walimu wengi wenye utaalamu wa lugha ya
ishara. Matokeo yake wale wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wanaachwa
nyuma bila kuelewa na hatimaye kufeli masomo yao.
Shule
Direct ilitambua umuhimu wa kutafuta mifumo mingine ya kuwasaidia
wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia, kuweza kujifunza. Masomo yakiwa
ndani ya Kompyuta ni rahisi kwa mwanafunzi huyo kusoma na kujifunza
katika kasi yake na kulingana na uelewa wake.
Hivyo,
Shule Direct ikaazimia kushiriki mbio za Kili Marathon 2016 ili
kuchangisha fedha kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Moshi Technical na
Njombe Shule ya Sekondari ya Viziwi (Shule pekee ya Sekondari ya viziwi
Tanzania). Fedha hizo ni kwa ajili ya kuwapatia ‘Content Lab’ kila
shule. ‘Content Lab’ inakuwa na kompyuta 20, masomo tisa ya Shule Direct
yaliyotengenezwa kwa mujibu wa ‘Syllabus’ ya Tanzania yanayowekwa moja
kwa moja kwenye kompyuta hizo kurahisisha upatikana ji bila ‘internet’
na kamusi ya lugha ya ishara ya signwiki.
Tarehe
27 Februari 2016, Mgeni rasmi, Afisa Elimu wa Manispaa ya Moshi Bw. Deo
Tulo Fundi akiwa na Afisa Elimu wa Elimu ya Mahitaji maalumu wa
Manispaa ya Moshi, Bi. Joyce Sawuo walishuhudia awamu ya kwanza ya
utoaji wa vifaa hivyo katika Shule ya Sekondari ya Moshi Tech.
Kabla
ya makabidhiano hayo, timu ya ufundi ya Shule Direct iliweza kutoa
mafunzo ya namna ya kutumia nyenzo hizo kwa walimu na wanafunzi wa Moshi
Technical, hususan wale walimu wanaosimamia wanafunzi wenye ulemavu.
Wakitoa
shukrani zao za dhati wakiongozwa na Mwalimu Mkuu wa Moshi Tech Mwl.
Erasmus Kyara na Mwalimu msimamizi wa anayesimamia mafunzo ya wanafunzi
wenye ulemavu walielezea furaha yao kupata kompyuta hizo zenye nyenzo za
kujifunzia, walisema kwa kipindi kirefu sasa wanafunzi wenye ulemavu wa
kusikia wamekuwa wakiwasindikiza tu wenzao kwa maana matokeo yao huwa
hayavuki daraja la nne, wanakumbuka kwa jina, mwanafunzi mmoja tu mwenye
ulemavu wa kusikia aliyewahi kupata daraja la tatu katika shule hiyo.
Akiongea
kwa niaba ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia shuleni hapo,
mwanafunzi wa kidato cha nne, Raphael, alielezea furaha yake kuwa
wanafunzi wenye tatizo kama lake wameweza kupatiwa msaada wa kompyuta
zenye masomo zitakazowawezesha kujisomea na kuelewa masomo yao zaidi,
alishukuru sana kupata nafasi ya kupata mafunzo ya vitendo ya jinsi
kutumia kompyuta hizo, zaidi alishukuru kwa fursa ya pekee ya
kukutanishwa na mwanadada Aneth Gerana ambaye aliongozana na timu ya
Shule Direct. Aneth ni mtanzania wa kwanza mwenye ulemavu wa kusikia
aliyefanikiwa kupata shahada ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam, naye ni
miongoni mwa wadau waliojitokeza kujiunga na Shule Direct katika zoezi
hili kwa kuwashirikisha wanafunzi maisha yake na kuwaasa kuwa wafanye
bidii katika masomo yao ili waweze kufaulu katika maisha.
Zoezi
la kusaidia wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia la Shule Direct
lililopatiwa jina la #KiliShuleThon 2016 lilifanikishwa kwa kiasi
kikubwa sana na mchango wa wadau mbali mbali wa elimu na maendeleo
waliojitokeza kuchangia, pia zoezi hili liliwezeshwa kwa mchango mkubwa
na ushirikiano na waandaaji wa Kili Marathon, Benki ya NMB, Freedom
Computers Limited na Lensmark Studios.
Post a Comment