Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Rais wa TWA Irene Kiwia kuhusu uzinduzi wa kampeni ya usawa wa kijinsia katika mkutano uliofanyika mapema leo Jijini Dar es salaam . |
Dar es Salaam, Februari 17, 2016: Taasisi ya TANZANIA WOMEN OF ACHIEVEMENT (TWA) imetangaza uzinduzi wa kampeni ya uwiano wa kijinsia kwenye kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani ya Wanawake inayotoa wito kwa kila mtu kuchukua hatua za dhati kusaidia upatikanaji wa usawa wa jinsia kwa kasi zaidi ili kuwasaidia wanawake na wasichana kufikia malengo yao.
Hali kadhalika inatoa wito kwa jamii kuwa na uongozi ulio na usawa wa kijinsia, kuheshimu na kuthamini tofauti bainia ya jinsia, kuanzisha utamaduni jumuishi na kuondoa upendeleo kwenye sehemu za kazi.
Akizungumza leo kwenye mkutano wa waandishi wa habari kwenye ofisi za TWA jijini Dar es Salaam Rais wa TWA, Bi. Irene Kiwia alisema kuwa lengo la Kampeni ya Uwiano wa Kijinsia ni kutoa wito kwa wanawake na wanaume kuungana pamoja kusaidia wanawake kufikia hali ya usawa kwa idadi kubwa na kutambua mchango wao usio na ukomo wanaoutoa kwenye uchumi duniani kote kwa ujumla hususani nchini kwetu Tanzania.
“Kampeni ya Uwiano wa Kijinsia inamaanisha kutoa wito kwa wadau wote vikiwemo vyombo vya habari, watu binafsi, serikali na mashirika yote kutambua na kujenga uelewa kuhusu mianya inayozuia mchakato wa kuwepo usawa wa kijinsia na kutaka kuchukua hatua za dhati kuharakisha mabadiliko,” alisema Kiwia.
“Mwaka 2014 Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum -WEF) lilitabiri kuwa usawa wa jinsia duniani utafikiwa mwaka 2095. Lakini mwaka mmoja baadaye, yaani 2015 lilikadiria kuporomoka kwa hatua husika na kupunguza kasi ya kufikia uwiano kuwa pengo la kijinsia linaweza kuzibwa ifikapo mwaka 2133. Hii inamaanisha kusubiri kwa miaka 117 ambayo ni mingi sana. Kutokana na hali hiyo TWA inaungana na wito wa dunia wa kuitaka kila nchi kuliweka suala la jinsia kwenye ajenda zake na kuharakisha kasi ya kufikia lengo la usawa wa kijinsia .” alisema Kiwia.
Akitoa wito kwa watu binafsi, mashirika na wadau wengine kushiriki kwenye kampeni hiyo Mwenyekiti wa TWA Bi. Sadaka Gandi alisema Kampeni itahusisha matembezi ya kilomita sita asubuhi ya siku ya tarehe Tano mwezi March kuanzia kwenye `Viwanja vya Mbio za Mbuzi´ maarufu kama ‘Uwanja wa Farasi’ kupitia kwenye makutano ya Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), kuelekea Kanisa Katoliki la Mt. Petro na kupitia Ubalozi wa Kenya nchini na kurudia sehemu yalipoanzia.
Bi. Sadaka Gandi aliendelea kusema kuwa matembezi hayo yatafuatiwa na mkutano wa kusherehekea siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ambao utafanyika Machi 6, 2016 kwenye Hoteli ya Regency Kilimanjaro.
Bibi Gandi alisema, “Mkutano huu utawakutanisha wanawake na wanaume kutoka sehemu tofauti ambao watashirikiana na kushawishiana kuungana na harakati hizi, vile vile tutaonyesha mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa kutoka Mkutano wa Beijing miaka 21 iliyopita, na hali kadhalika ni kasoro gani ambazo bado zipo na ni kwa namna gani ushirikiano wa pamoja unaweza kuharakisha mabadiliko. Tunaamini mchango wako sio tu kwamba utachangia msingi wa maendeleo ya wanawake bali pia utaonesha ni jinsi gani kampuni yako inachangia kwenye upatikanani wa usawa wa kijinsia kwa ujumla”.
Bibi Gandi alisema kuwa mkutano huo utazungumzia masuala mbalimbali yanayomhusu mwanamke kwa kuzingatia elimu, afya, uongozi, haki na sheria na uchumi.
“Usawa wa jinsia ni muhimu kwa sababu umefungamana na kukua kwa uchumi kwani maendeleo ya wanawake na uongozi ni nguzo ya ufanisi kwenye biashara na ustawi wa uchumi”, alihitimisha.
Post a Comment