ALIYEKUWA mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) visiwani
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka Wazanzibari na wapenda
amani kuondoa shaka na kwamba, atatangazwa kuongoza visiwa hivyo.
Anaandika Mwandishi Wetu.
Maalim Seif ametoa kauli kwenye viwanja vya Nngoma Hazingwa, Chake Chake
Pemba akiwa na viongozi wa wilaya, majimbo na jumuiya za chama hicho
ikiwa ni siku moja baada ya kufanya mkutano wa namna hiyo Unguja.
Kiongozi huyo ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF amesema kuwa, ukweli
umedhihiri ndani na nje ya nchi na kwamba hakuna sababu ya kutotangazwa
kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana.
Amesema, “jumuiya na waangalizi wote wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa
wameshuhudia uchaguzi huo na kujiridhisha kuwa ulikuwa huru, haki na wa
uwazi na wanaendelea kushikilia msimamo wao kutaka mshindi wa uchaguzi
huo atangazwe.”
Amesisitiza kuwa CUF haitoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa
kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu kauli ambayo pia imeungwa mkono na
wafuasi wa chama hicho Pemba kama ilivyokuwa Unguja.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amemtaja
Maalim Seif kuwa kiongozi aliyebobea kisiasa na anayejali maslahi ya
Wazanzibari.
Katika hatua nyingine mawakilishi na madiwani wateule wa CUF kupanga kwenda mahakamani kutetea nafasi zao.
Wameeleza kwamba, kwa kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imewapa hati
za ushindi baada ya kufanya uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba 2015, mpaka
sasa hakuna aliyejitokeza kupinga ushindi wao.
Hata hivyo, Maalim Seif amesema, viongozi hao waliochaguliwa na wananchi
katika uchaguzi huo na kisha kupewa shahada zao, watakwenda mahakamani
kutetea nafasi zao na kutoruhusu viongozi wengine wa ngazi hizo
kuchaguliwa tena kwa vile wao wanavyo vielelezo vyote vya kuchaguliwa
kwao.
Post a Comment