Mwenyekiti
wa Mfuko wa Doris Mollel Foundation, Bi. Doris Mollel akiwakaribisha
wageni mbalimbali na wanahabari wakati wa utambulisho maalum juu ya
tamasha linalotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili Novemba 8, katika
viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Kaimu
Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, uzazi na watoto, Bi. Georgina Msemo na
kulia kwake ni Dk. Sonal Peter ambaye ni daktari wa watoto
(Pediatrician) kutoka Hospitali ya Agha Khan. (Picha zote na Andrew
Chale, Modewjiblog).
Na Andrew Chale, Modewjiblog
[DAR
ES SALAAM] Katika kuadhimisha siku ya watoto njiti duniani, Taasisi ya
Doris Mollel Foundation (DMF) imeandaa tamasha la kwanza na la aina
yake kufanyika nchini siku ya Jumapili Novemba 8. 2015 kwenye viwanja
vya Leaders Club, Kinondoni kuanzia majira ya asubuhi mpaka saa 12 jioni
huku wasanii mbalimbali wakitarajiwa kushiriki kwa ajili ya kuchangisha
fedha za kununulia vifaa vya kusaidia watoto wanaozaliwa na uzito
pungufu ama watoto njiti.
Akielezea
mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam mapema jana, dhumuni la
tamasha hilo ni kuwaleta watanzania pamoja kupata uelewa na mwamko
katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa afya na ustakabali wa mtoto
njiti ambapo kulingana na takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
takribani watoto 88,128 walizaliwa njiti au wakiwa na uzito mdogo nchini
kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 pekee.
“Lengo
ni kuhakikisha kupitia Mfuko huu unasaidia watoto njiti hasa kwa vifaa
vya kuwawezesha kusaidia maisha yao. Tunataka kufikisha vifaa 10 kwa
kila Kanda chache za awali. Karibuni sana watanzania kwa siku ya
Jumapili Novemba 8. Kwa kiingilio cha sh 2,000 pekee kama mchango
ambapo utapata burudani ya kipekee kutoka kwa wasanii mbalimbali
wakiwemo Barnaba Classic, Mwasiti, kundi la The Voice, Miriam, Baraka De
Prince, Ruby, Shilole na wengine wengi.” Amebainisha Doris Mollel.
Aidha,
Doris amebainisha kuwa, Watanzania watapata fursa maalum ya kuusikia
wimbo ulioimbwa na baadhi ya wasanii hao watakaoshiriki katika tamasha
hilo.
DMF
imeongeza kuwa, baada ya tamasha hilo, kwa kushirikiana na wadhamini
pia itatoa vifaa mbalimbali ikiwemo (Suction machines, Oxygen
Concentrators na Feeding tubes) hii ni kwa Hospitali za Mikoa nchini
ilikuweza kusaidia watoto hao na vifaa hivyo vinatarajiwa kutolewa
katika siku ya kilele cha maadhimisho ya mtoto njiti Duniani huku kwa
Tanzania ikitarajiwa kufanyika Mkoani Mbeya.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, Uzazi na Watoto, Bi.
Georgina Msemo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo amezitaka jamii nchini
kujitokeza kwa wingi kusaidia wamama wajawazito wakati wa kipindi chote
cha ujauzito kwani kusaidia huko kutapunguza watoto wanaozaliwa kabla ya
wakati ama njiti.
“Jamii
iwe na huruma kwa wamama wajawazito. Kwani haya yote yanatokea
kutokana na wamama wengi wanakuwa wanafanya kazi ngumu kutopatiwa huduma
muhimu na hata wengine kutokwenda kliniki… hivyo ni jamii ichukue
hatua ya kusaidiana na wajawazito kutatua tatizo hili” alieleza Bi Msemo
katika taarifa yake hiyo aliyoitoa wakati wa hafla hiyo ya utambulisho
wa tamasha la kuchangia fedha za kusaidia watoto njiti.
Wajue Watoto njiti:
Watoto
wanaozaliwa kabla ya muda wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kufa
kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa, mfumo wa chakula na mfumo wa
fahamu ukilinganisha na watoto waliozaliwa baada ya kutimiza wiki 37 au
zaidi wakiwa tumboni mwa mama zao. Watoto njiti pia wapo katika hatari
ya kupata matatizo ya kuona, kusikia, kutambua/kiakili na moyo
yanayoweza kudumu maisha yao yote. Zaidi ya hapo watoto wanaozaliwa
njiti katika nchi zilizo na uchumi duni wapo katika hatari ya kufa mara
10 zaidi ukilinganisha na watoto njiti wanaozaliwa katika nchi
zilizoendelea
Tukio hilo likiendelea.
Tunaweza kupunguza idadi ya njiti
Sababu
kuu zinazosababisha hali ya hatari kwa watoto njiti nchini Tanzania na
nchi nyingine zenye uchumi mdogo ni maambukizi wakati wa ujauzito,
Malaria, VVU, kuzaliwa na uzito mdogo, muda mfupi kati ya uzao mmoja na
mwingine na mimba za utotoni. Matunzo sahihi kabla, katikati na wakati
wa ujauzito (ikiwemo uzazi wa mpango na huduma wakati wa ujauzito) ni
muhimu katika kupunguza kiwango cha uzazi wa watoto njiti. Hata hivyo
sehemu kubwa ya sababu zinazofanya watoto kuzaliwa njiti hazijulikani.
Hivyo basi tunahitaji kufanyike tafiti zaidi ili kupata uelewa na
kudhibiti visababishi vyake.
Tunaweza kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaokufa kutokana na matatizo ya kuzaliwa njiti
Mtoto
anayezaliwa njiti sio lazima apewe uangalizi wa karibu (intensive care)
na kutumia teknolojia kubwa sana ili aishi. Huduma za gharama nafuu
zinazoweza kufanyika ili kuongeza uwezekano wa mtoto mchanga kuishi na
kupunguza hatari kwake ya kupata ulemavu wa maisha, ni pamoja na
zifuatazo:
1.Antenatal steroids, hizi
ni dawa ambazo hutolewa kwa akina mama wanapopata uchungu wa kujifungua
kabla ya wakati, katika ngazi za afya zinazostahili, husaiidia kukuza
mapafu ambayo hayajakomaa ya mtoto njiti na kuzuia matatizo kwenye mfumo
wa hewa ya watoto wachanga.
2.Huduma ya Mama Kangaruu: Hii
ni mbinu ya kumbeba mtoto mchanga kwenye kifua cha mama yake wakigusana
ngozi kwa ngozi ili kumpa joto na kurahisisha unyonyeshaji. Ni muhimu
kuwapatia joto watoto njiti kwa sababu miili yao ni midogo na hupoteza
joto haraka, jambo linalowafanya kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata
magonjwa mbalimbali, maambukizi na kifo. Inakadiriwa kuwa mbinu hii ya
Mama Kangaruu inaweza kuepusha vifo vya watoto 5,000 kila mwaka hapa
Tanzania.
Baadhi ya wasanii waliokuwapo wakati wa utambulisho huo wakifuatilia kwa makini.
3. Kusaidia watoto kupumua kwa kutumia bag na mask, ni
huduma muhimu kwa watoto njiti wenye matatizo ya kupumua. Iwapo huduma
hii rahisi ya kusaidia watoto wachanga kupumua inapatikana kwa asilimia
90 ya watoto wanayoihitaji, basi takribani maisha ya watoto wachanga
2,000 yangeweza kuokolewa kila mwaka. Mpango wa Kusaidia Watoto Kupumua
(Helping Babies Breathe) ulizinduliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii mwaka 2009 kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya
katika ngazi zote, ukiwa na lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga
vinavyotokana na matatizo ya kupumua. Wadau wa afya mbalimbali
wameshirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kutekeleza
mpango huu.
4.Kumsaidia mama kuanza kunyonyesha mtoto ndani ya saa moja baada ya kujifungua, hii inahusisha pia kumsaidia mama kukamua maziwa kwa ajili ya mtoto na kumpa kwa kutumia kikombe pale inapo lazimu.
5.Kuzuia, kutambua mapema na kutibu maambukizi: utoaji
wa huduma inayozingatia usafi wakati wa mama kujifungua (mfano kuosha
mikono, uhudumiaji sahihi wa kitovu na ngozi ya mtoto mchanga) ni muhimu
katika kuzuia maambukizi kwa mama na mtoto. Dawa za antibiotiki kama
vile Amoxicillin zinaweza kutumiwa kutibu nimonia na Gentamicin kwa
ajili ya kutibu maambukizi makubwa yanayowapata watoto wachanga.
Zaidi
ya hapo, watoto wote wachanga wanahitaji kukaguliwa afya zao ndani ya
masaa 24 na baada ya siku 3 ya kuzaliwa ili kuzuia matatizo yanayoweza
kutokea na yale ambayo yanaweza kusababisha ulemavu katika maisha yao ya
baadaye.
Huduma bora inahitajika wakati wa kujifungua na hususan kwa watoto wachanga wanaozaliwa na uzito mdogo na wale walio wagonjwa.
Baadhi ya waashiriki hao katika mkutano huo.
“Watoto
wachanga wanahitaji kupata huduma muhimu hususan kwa wale ambao
wanazaliwa kabla ya muda wao,” anasema Mwakilishi wa Unicef nchini
Tanzania Dk. Jama Gulaid.
DMF imetoa pia nafasi ya wazi kwa watanzania kuchangia kiasi chochote kile kupitia M-PESA namba ya kampuni 244444 (Doris Mollel Foundation).
Jinsi ya kuchangia kwa M-Pesa: (1) Piga *150*003# chagua lipa kwa M-pesa (2) Weka namba ya kampuni ambayo ni 244444. (3)
Weka kiasi (mfano: Tsh.500, 3200, 7000 na kuendelea kadri ya uwezo wa
mchangiaji. (4) Weka namba ya kumbukumbu ambayo ni (2015). Kisha
utaweka namba yako ya siri ya M-Pesa (PIN yako ya MPESA) na kisha
utabonyeza namba moja kuthibitisha muamala wako na baadae utapokea
ujumbe wa maandishi (SMS) kwamba umechangia Doris Mollel Foundation
kwenye akaunti michango ya mwaka 2015. (Unaweza kuchangia kiasi chochote
mara nyingi uwezavyo.
Aidha, DMF imewashukuru wadhamini mbalimbali wanaoendelea kufanikisha shughuli za kusaidia harakati hizo ikiwemo Vodacom
Foundation, Clouds Media Group, Hyatt Regency, NSSF, CBA, NHIF, Coca
Cola, Moments productions, Ashton Media, Expo Trading, Viva towers Easy
talk, SpiceNet, MillardAyo.com, Modewjiblog na wengine wengi.
Dk.
Sonal Peter ambaye ni daktari wa watoto (Pediatrician) kutoka Hospitali
ya Agha Khan akielezea namna ya kuchangia Mfuko huo na kuhamaisha Jamii
kujitokeza kwa wingi.
Wasanii
wa kundi la The Voice, Barnaba Classic na wengineo wakiimba kwa hisia
wimbo maalum wa kumpa matumaini Mama mjamzito na aliyejifungua mtoto
njiti katika kusaidia maisha yake.
Bi.
Doris Mollel akiwapongeza wasanii hao kwa kumuunga mkono katika tukio
hilo likiwemo la kuimba wimbo maalum na pia kutumbuiza siku ya Jumapili
Novemba 8.2015.
Mtangazaji wa Chaneli Ten, Said Makalla akiuliza swali kwa Mwenyekiti wa Doris Mollel Bi Mollel (hayupo pichani).
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, Uzazi na Watoto, Bi. Georgina Msemo
(kushoto) akijibu swali la Said Makalla (hayupo pichani).
Kundi la The Voice wakiimba wimbo huo ambapo baadhi ya sehemu walizorekodia ni kwenye wodi ya watoto njiti.
Post a Comment