Ikiwa zimebaki siku 23 kufikia siku ya kupiga kura nchini, mapya yameibuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, akidai kuwa zipo njama chafu za kumdhuru na kutengeneza ushahidi wa video na picha mnato na kuzisambaza.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbatia alidai kuwa
njama hizo alizozigundua zilipangwa katika mikakati tofauti na
kuhakikisha zinafanikiwa.
Alitaja mbinu ya kwanza iliyopangwa kutumika kuwa ni kumteka akiwa anaelekea nyumbani kwake au mahali popote.
Mbinu ya pili alidai
kuwa ni kuwapandikiza na kuwavisha vijana sare za Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), ambao wangemvamia mahali popote, wamteke na
kumjehuri ili ionekane kuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), kuna mgogoro.
Ya tatu kwa
mujibu wa Mbatia, ni kuwakusanya wajumbe wa chama chake na wanachama
kwa pamoja ili waende kumfukuza kwenye Chama, kwa madai ya kutotekeleza
majukumu yake ipasavyo.
Mbatia alidai kuwa mpango huo ulikuwa ukiratibiwa na Makamu wa Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi (Tanzania Bara), Leticia Mosore, kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Makamishna wa chama hicho taifa, Peter Mushenyela.
Alidai
kuwa jama hizo zilipagwa Septemba 19, mwaka huu, kwa kumtumia fedha na
tiketi ya ndege, Mushenyela aliyekuwa mkoani Kagera ili aje jijini Dar
es Salaam kumsaidia Musore kutekeleza mpango huo.
Hata
hivyo, Mbatia alidai kuwa Mushenyela alikataa kushiriki mpango huo na
kuamua kwenda kutoa taarifa Jeshi la Polisi ambalo walifungua jalada
namba KW/RB/9600/2015 siku hiyo hiyo.
Kwa
mujibu wa Mbatia, mbali ya Mosore kutuma fedha za nauli kwa Mushenyela,
pia alituma fedha kwa wajumbe kadhaa wa mikoa wa chama hicho ili
kuwashawishi waingie katika mpango huo wa kumdhuru.
Alidai kuwa Mwenyekiti huyo wa Makamishna naye aliwasiliana na naye (Mbatia) ambapo walishauriana kuweka mtego.
Alidai
kuwa mpango huo wa kumdhuru, uliwashirikisha Makamishna wanne wa chama
hicho wanne ambao waliletwa jijini Dar es Salaam na kuhifadhiwa katika
hoteli moja huku wakilipwa posho ya kujikimu Sh. 60,000 kwa siku.
"Fedha
hizo zilikuwa zinalipwa na watu wa chama kingine cha
siasa...(akikitaja), ambao walikuwa wakishirikiana na Musore, huku
wakiendelea na mipango yao ya kunidhuru, kuvuruga chama changu, Ukawa na
viongozi wake kwa ujumla," alidai Mbatia.
“Mimi
baada ya kupata taarifa zile kutoka kwa Mwenyekiti wa Makamishna kwamba
Makamu Mwenyekiti anapanga mikakati hiyo na anataka ashirikiane naye,
nilimwelekeza namna ya kujipanga ili kubaini njama hizo," alidai.
Pia
Mbatia alida kuwa Septemba 17, mwaka huu, Mosore aliitisha kikao na
waandishi wa habari kinyume na Katiba ya chama na kuzungumza mambo ya
chama ambayo hayakuwa na baraka za Chama.
Alidai
kuwa katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, Mosore alimtuhumu
yeye (Mbatia) kuwa amekidhoofisha na kutelekeza chama na kwamba
amewekeza nguvu zaidi Ukawa na kujifanya Msemaji wa Chadema.
Hata hivyo, Mbatia alidai kuwa Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi iliyokutana Septemba 22, mwaka huu, iliamua kumsimamisha Mosoreuongozi bila kumpa barua kwa kuwa uchunguzi ulikuwa unaendea.
“Si kwamba Makamu Mwenyekiti tumemsimamisha tu, lakini pia anashtakiwa kwa kupanga njama za kutaka kunidhuru," alisisitiza Mbatia.
Kwa
upande wake,Mwenyekiti wa Makamishna wa chama hicho, Mushenyera alisema
pamoja na kulipwa fedha za kujikimu kila siku, pia waliahidiwa kupatiwa
Sh. milioni 10 kila mmoja endapo wangesoma hadharani na kurusha moja
kwa moja waraka ambao ulikuwa umeandaliwa na Mosore na watu wa chama
kingine wa kuwachafua yeye Mbatia, mgombea Urais wa Chadema, Edward
Lowassa na Ukawa kwa ujumla.
Hata
hivyo, Mushenyela alikataa kutaja majina ya watu wa chama kingine kwa
madai kwamba ni hatari kwa maisha yake kwa kuwa ni wana fedha nyingi
wanaweza kumdhuru.
Hata
hivyo, Mosore alipoulizwa kuhusiana na madai hayo ya Mbatia,
alikanusha vikali akidai kuwa tangu alipozungumza na waandishi wa habari
Septemba 17, mwaka huu na kutoa yake ya moyoni, hajawahi kushiriki ama
kupanga njama zozote za kumdhuru Mbatia.
Kuhusu suala la kusimamishwa nafasi ya uongozi, Mosore alisema:
“Mimi
sijui kama nimesimamishwa na kwanza ndiyo napata taarifa kutoka kwako
na kama wangekuwa wamenisimamisha, wangenipa barua,” alisema Mosore.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura,
alithibitisha kupokea ripoti ya Mbatia kuhusiana na madai yake ya kutaka
kumdhuru.
Post a Comment