Ndugu waandishi wa habari;
Tumewaita hapa kuwaomba muwaeleze Watanzania wenzetu, jumuiya ya kimataifa na marafiki zetu wengine wa ndani na nje, kwamba hatukubaliani na matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais, yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kote nchini.
Hii ni kwa sababu, upo ushahidi wa wazi unaothibitisha kwamba utangazaji wa matokeo hayo umevurugwa kwa makusudi na watendaji ndani ya NEC kwa kusaidiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika maeneo mengi ambako matokeo yameshatangazwa mpaka sasa, kilichoripotiwa kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais, hakifanani wala kuendana na matakwa halisi ya wananchi.
Matokeo mengi yamesheheni udanganyifu, ulaghai na yameandaliwa kwa lengo maalum la kumbeba mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli.
Katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi, kura zetu zimepunguzwa na kuongezwa kwa mgombea wa CCM; maeneo mengine, kura zilizotangazwa zimetofautiana na idadi halisi ya kura zilizopigwa.
Kwa mfano, matokeo yaliyotangazwa na NEC katika majimbo ya Mkoani na Mtambile, kisiwani Pemba, Makunduchi, Kiwengwa, Donge, Tunduru, Tunduma, Same Mashariki, Chambani, Tandahimba, Kilindi na kwingi kwingineko, ni miongoni mwa matokeo yanayothibitisha kuwa hiki kinachotangazwa na NEC, siyo kura za uchaguzi mkuu wa rais. Tunaweza kuiita, “mzimu wa uchaguzi.”
Ndugu waandishi wa habari;
Tangu kuanza kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi huu, viongozi wetu wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) – mimi mwenyewe juzi na jana Mhe. Freeman Mbowe, James Mbatia na Profesa Abdallah safari walilieleza kasoro zilizojitokeza katika matokeo ya rais,
Hata hivyo, Tume imeendelea kutangaza matokeo hayo, bila kujali kile ambacho tumekieleza na kukilalamikia, kana kwamba tunachokisema ni ujinga, uzushi na uwendawazimu. Hili halikubaliki.
Aidha, katika maeneo mengine, likiwamo jimbo la Ubungo, matokeo yaliyoko mikononi mwa msimamizi wa uchaguzi, yanatofautiana na yale ambayo yamekusanywa kutoka katika vituo vyote vya jimbo hilo.
Hali kama hiyo ipo pia katika majimbo yote ambayo wagombea wa CHADEMA na wale wa vyama washirika vya CUF na NCCR – Mageuzi, ama wamekuwa na nguvu kubwa au wameibuka washindi.
Upo ushahidi wa wazi ambao, ninyi waandishi mnaweza kwa kutumia uandishi wenu kuuthibitisha kwamba, katika majimbo yote ambako wagombea wa UKAWA wameshinda, TUME imechelea kutangaza matokeo ya urais kwa sababu zinazothibitisha kuwapo kwa mikakati ya hila.
Ikumbukwe kwamba matukio yote haya ya NEC kutangaza matokeo yaliyochakachuliwa yamekuja baada tu ya Jeshi la Polisi kuvamia vituo vyetu vitatu vya kuhesabia kura na kuwakamata wataalam wetu waliokuwa wakipokea matokeo ya kura za rais nchi nzima ambayo hadi uvamizi huo ulipofanyika tulikuwa tukiongoza katika maeneo mbalimbali.
Ndugu waandishi wa habari;
Tunaamini kwa dhati kwamba, uvamizi huo ulifanyika mahususi kwa malengo ya kufanikisha uchakachuaji huo ambao sasa tunauona ukiendelea kufanyika kupitia matangazo yanayoendelea kutolewa sasa na NEC.
Wakati tukijua kwamba NEC ndiyo mamlaka pekee ya kisheria ya kutangaza matokeo ya urais, tunapenda kuwataarifu Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwamba hadi wakati uvamizi huo ulipofanyika kura zetu za urais tulizokuwa tumezikusanya zilikuwa zikionyesha tukiongoza kwa asilimia zaidi ya 60.
Kutokana na makosa hayo makubwa na ya makusudi yanayofanywa na watendaji wa NEC, mimi Edward Ngoyai Lowassa, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji, tunautangazia umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa, kwamba hatukubaliani na matokeo yanayotangazwa na NEC.
Ndugu waandishi wa habari;
Kutokana na makosa hayo makubwa, tunaitaka NEC kusitisha mara moja utangazaji wa matokeo ya urais na kuanza upya kufanya uhakiki wa kile wanacholetewa na wasimamizi wa majimbo ambacho ushahidi unaonyesha kuwapo kwa vitendo vya hila ambavyo vinafanywa na NEC.
Ndugu wana habari
Kile kinachofanywa na NEC hapa ndiyo kile kile kinachoendelea kufanywa kule Zanzibar leo na ZEC ambako kunafanyika juhudi kubwa na za makusudi kupora kwa hila na kwa mabavu mwelekeo wa wazi wa ushindi wa Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF anayeungwa mkono na UKAWA, Maalim Seif Sharif Hamad.
Post a Comment