PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Tusikubali kuligawa Taifa kwa misingi ya dini
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Jambo hili liliwezekana, kutokana na misimamo thabiti ya waasisi wa Taifa hili, kukemea hadharani watu ambao walitaka kuligawa Taifa. ...
Jambo hili liliwezekana, kutokana na misimamo thabiti ya waasisi wa Taifa hili, kukemea hadharani watu ambao walitaka kuligawa Taifa.

NA: MUSSA JUMA

Waasisi wa Taifa la Tanzania, walifanikiwa kujenga misingi imara ya kutowagawa Watanzania katika misingi ya dini, makabila na rangi.
Jambo hili liliwezekana, kutokana na misimamo thabiti ya waasisi wa Taifa hili, kukemea hadharani watu ambao walitaka kuligawa Taifa.
Ingawa ni kweli kuwa, huwezi kutenga dini na siasa, pia kwa Taifa lenye wananchi wenye dini na madhehebu tofauti kama Tanzania, kutumia msingi wa dini moja pekee kuamua jambo ni hatari.
Nasema ni hatari kwa sababu, haiwezekani waumini wote wa dini zote wakakubaliana na jambo ambalo limeshinikizwa na dini moja, labda jambo hilo liwe na masilahi kwa dini moja.
Kwa muktadha huu, nataka kuzungumzia kidogo waraka wa Maaskofu kuhusu Katiba Inayopendekezwa ambao tayari umeanza kusomwa kwenye makanisa mbalimbali nchini.
Waraka huu wa kitume, licha ya kuwa na maudhui ambayo yanaungwa mkono na Watanzania wengi, kuelekeza waumini wa Kikristo kutoipigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa, nadhani kuna tatizo.
Ni ukweli ulio wazi kuwa kuna maelfu ya waumini wa dini nyingine, wanaunga mkono maudhui ya waraka huu, lakini kwa kuhimiza Wakristo pekee kupiga kura ya hapana ni kuligawa Taifa.
Shinikizo la Maaskofu wetu, ni wazi kwa siasa zetu litaibua baadhi ya viongozi wa dini nyingine nao kusimama na kuwataka waumini wao waipigie kura ya ndiyo Katiba na hata tutakuwa tumekwisha.
Fikiria mchakato wa kampeni ya kupigia kura Katiba ukianza kuongozwa na viongozi wa dini, hali itakuwaje?

Hapa tutegemee uhasama mkubwa na baadaye kuligawa Taifa kwa misingi ya dini, binafsi namwomba Mungu atuepushie kikombe hiki.
Busara hizi za Kardinali Pengo zinapaswa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote, kuacha kutumia mamlaka yao ya kiimani kushinikiza jambo ambalo linahitaji ridhaa ya wananchi wote bila kujali dini zao.
Watanzania wengi wanaipinga Katiba Inayopendekezwa lakini ni vyema kutumia njia sahihi kutaka wananchi wapige kura ya hapana na hakika wengi watashinda hata kama zoezi la kura likigubikwa na mchezo mchafu.
Nawakumbusha uchaguzi mkuu mwaka 2000, baadhi ya viongozi wa chama tawala, walikuwa wanapiga kampeni chafu wakati huo wakisema CUF kilikuwa Chama cha Waislamu hivyo kisipigiwe kura.
Walifanikiwa kuwadanganya wananchi hasa wa vijijini lakini walifanikisha kukijenga Chama cha CUF hasa katika maeneo yenye Waislamu wengi.
Haikuishia hapo uchaguzi wa mwaka 2010 baadhi ya viongozi hawa hawa, waliibuka na kuendesha kampeni kuwa, Chadema ni Chama cha Wakristo na walifanikiwa kuwadanganya wachache, pia walikiimarisha chama hicho.
Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa, kwa kawaida dhambi ya ubaguzi ikianza, husambaa na sasa inasambazwa kwa kasi na viongozi hawa waliotufikisha hapa. Leo wapo kimya wakati maaskofu wakitoa waraka wao.
Naamini wapo kimya kwa sababu wanajua wao ndiyo waasisi wa siasa hizi za udini na wameshindwa kufanya uamuzi sahihi wakati wote, kwa kuzingatia misingi ya dini zao na kutetea masilahi yao ya kisiasa.
Kwa mfano, suala la Mahakama ya Kadhi ni viongozi hawahawa, baada ya malalamiko ya Waislamu kwa muda mrefu, waliweka kwenye ilani yao kuwa wakishinda watarejesha Mahakama za Kadhi, lakini kwa kuwa hawakuwa na dhamira za dhati na walilenga masilahi ya kisiasa hadi leo suala hili limekuwa hadithi.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top