Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, jana ilimsulubu Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ikieleza kuwa wizara yake iliingia mkataba wa mradi wa treni za kisasa kutoka Stesheni ya Dar es Salaam hadi Pugu kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) bila kufuata taratibu.
Kambi hiyo ililieleza Bunge kuwa mkataba huo
ulisainiwa baina ya mmiliki wa Kampuni ya M/s Shumoja, Robert Shumake na
Shirika la Reli Tanzania huku Waziri Mwakyembe akishuhudia.
Msemaji Mkuu wa kambi hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Uwekezaji na Uwezeshaji, Pauline Gekul alitoa madai hayo wakati
akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu muswada wa marekebisho ya Sheria
ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).
Gekul alisema taratibu hazikufuatwa kwa kuwa
haieleweki ni lini Serikali, wakala au Wizara ya Uchukuzi ilitangaza
zabuni ya mradi wa treni kutoka Stesheni hadi Pugu kupitia JNIA.
“Pia haijulikani ni lini Serikali ilifanya
upembuzi yakinifu kuhusu mradi huo wa reli kwa kufuata taratibu kama
zinavyoainishwa na Sheria ya PPP ya mwaka 2010 ambayo inafanyiwa
marekebisho hivi sasa,” alisema Gekul na kuongeza: “Haijulikani ni
kampuni ngapi ambazo ziliomba tenda ya ukandarasi wa treni na kwamba M/s
Shumoja ilishinda tenda hiyo kwa vigezo gani.”
Alisema kwa kifupi ni wazi kuwa Dk Mwakyembe na
wizara yake walikiuka vifungu vya Sheria ya PPP. Alivitaja vifungu hivyo
kuwa ni 4(1) na (2) vinavyomtaka waziri kutangaza katika Gazeti la
Serikali miradi mbalimbali inayotegemewa kufanywa na sekta ya umma kwa
ubia na sekta binafsi.
Gekul alisema pia kifungu cha 5(1) kilikiukwa
ambacho kinaitaka mamlaka inayohusika kufanya upembuzi yakinifu baada ya
kupembua mradi ambao utafanywa kwa ubia.
“Pia kifungu cha 9 kinachotaka mzabuni kutoa
nyaraka mbalimbali za miradi ikiwamo jina, mahesabu yaliyofanyiwa
ukaguzi pamoja na vielelezo vya uwezo wa kifedha,” alisema Gekul.
Alihoji kulikuwa na uharaka gani wa utekelezaji wa
mradi huo ambao umekiuka Sheria ya PPP bila kuwahusisha wadau wengine
ambao wangeweza pia kushindana na Shumoja?
“Ingekuwa ni vyema kama Serikali ingeweka bayana
undani wa mkataba wa mradi huo ambao kama Watanzania hatujawahi kusikia
ukitangazwa ili kutoa fursa kwa wazabuni wenye uwezo kushindania zabuni
hiyo zaidi ya kuona na kuusikia mradi siku ya utiaji saini,” alisema.
Alisema Serikali ikishabanwa kutoa majibu juu ya
uvunjwaji wa sheria, huja na majibu ya kejeli, hivyo Watanzania waelewe
kuwa sheria zimekuwa zikipindishwa ili kupitisha miradi ambayo baadaye
hugeuka kuwa mzigo kwao kama ilivyokuwa IPTL na Escrow.
Alisema pamoja na adha ya usafiri jijini Dar es
Salaam, ukweli utabaki palepale kwamba, Dk Mwakyembe alisimamia mchakato
wa mradi uliokiuka sheria ambao ikiwa utashindikana katika utekelezaji
na mzigo wa uvunjwaji ama usitishwaji wa mkataba, gharama zitarudi kwa
Watanzania.
Post a Comment