Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana,
Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi,
Kharist Michael Luanda alisema wananchi wanaotaka kuwania nafasi
mbalimbali za uongozi katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa
wanapaswa kuchukua fomu za kugombea kuanzia Novemba 16 hadi 22.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuwachagua viongozi wanaowataka kwenye vijiji, vitongoji na mitaa.
Alisema uandikishaji huo utafanyika katika vituo
maalumu vilivyoandaliwa ambavyo vipo katika majengo ya umma kuanzia saa
1.30 asubuhi na kufungwa saa 10.30. Alisema katika sehemu ambazo hazina
majengo, uandikishaji utafanyika katika vituo maalumu kutokana na
makubaliano ya msaidizi wa uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa.
Alisema vyama vya siasa vitaruhusiwa kuweka
mawakala wakati wa uandikishaji wa wapigakura lakini gharama za kuwalipa
zitakuwa juu ya chama husika. Kuhusu sifa za anayetaka kuwania nafasi
katika ngazi hizo, mkurugenzi huyo alisema ni lazima awe Mtanzania
mwenye miaka 21 au zaidi na awe mkazi wa kudumu wa eneo husika.
Alisema wasimamizi wasaidizi wa kila kituo
wanapaswa kubandika orodha ya wapigakura ifikapo Novemba 30 na endapo
mkazi yeyote au chama cha siasa kitakuwa na pingamizi au maoni juu ya
orodha hiyo, awasiliane na msimamizi msaidizi wa uchaguzi ili kufanya
marekebisho na orodha ya mwisho itabandikwa siku tatu kabla ya uchaguzi.
Viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi wa
Serikali za Mitaa ni wajumbe wa halmashauri ya kijiji wasiopungua 15 na
wasiozidi 25, wenyeviti wa mitaa na wajumbe wa kamati za mitaa
wasioziidi sita na wenyeviti wa vitongoji.
Post a Comment