PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: RAISI KIKWETE ATOFAUTIANA NA JAJI WEREMA JUU YA KURA YA MAONI YA KATIBA MPYA
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
    Rais Jakaya Kikwete amesema endapo mipango yote itakwenda kama inavyoandaliwa, Watanzania wataipigia kura ya maoni Katiba Inayopend...
   

Rais Jakaya Kikwete amesema endapo mipango yote itakwenda kama inavyoandaliwa, Watanzania wataipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa Aprili mwakani.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete aliitoa jana alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China,

Kauli hiyo inapingana na ile ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania (AG), Jaji Frederick Werema ya hivi karibuni kwamba kura hiyo ingefanyika Machi 30, mwakani.

Mbali na Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva alisema juzi mjini Dodoma kwamba kura ya maoni haiwezi kufanyika Machi 30 mwakani kwa sababu kazi ya uandikishaji wa daftari la wapigakura haitakuwa imekamilika.

Rais Kikwete aliwaambia mabalozi hao kuwa mchakato wa Tanzania kusaka Katiba Mpya unakwenda vizuri baada ya kupitia hatua zote ikiwamo ile ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kuundwa kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi na Bunge Maalumu ya Katiba ambalo lilipigia kura ya kuipitisha Katiba Inayopendekezwa.

“Lililobakia sasa ni Kura ya Maoni ya Wananchi. Tunadhani kuwa kama itakwenda kama tulivyopanga, kura hiyo itapigwa wakati wowote Aprili mwakani. Bado tunaangalia tarehe mwafaka kwa ajili ya shughuli hiyo muhimu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Katiba hiyo ikipita, sote tutashangilia na kusherehekea lakini matokeo ya Kura ya Wananchi yakiwa tofauti, basi tutaendelea kuongozwa na Katiba ya sasa mpaka huko mbele wakati nchi yetu na wananchi watakapoamua tena kujaribu kupata Katiba Mpya.”

Jaji Lubuva
Akizungumza katika semina ya Baraza la Vyama vya Siasa mjini Dodoma, Jaji Lubuva alisema itakuwa vigumu kufanyika kwa kura hiyo Machi 30 kama ilivyotangazwa na Jaji Werema kwani kazi ya uandikishaji wa daftari la wapigakura imechelewa kuanza kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kukosekana fedha.

“Serikali imeshatuhakikishia itafanya malipo na kati ya sasa na Desemba baadhi ya vifaa vinaanza kuja. Malipo yakishafanywa katika miezi hiyo mitatu; Januari, Februari na Machi tutajitahidi kila iwezekanavyo kuboresha daftari.”

Jaji Lubuva naye alisisitiza kuwa Tume yake haitafanya uchaguzi au kura ya maoni kama daftari halijaboreshwa.

“Naona kuna gazeti moja (Mwananchi) lilisema Kura ya Maoni ni Machi 30 mwakani, haiwezekani. Tulisema Januari, Februari, Machi sasa unaposema Machi 30, mwezi Machi haujaisha kwa hiyo ni tarehe ambayo itakuja baada ya hapo,” alisema.
Alisema ikiwa mambo ya fedha yatakwenda kama alivyosema AG, Tume itajitahidi kwa kipindi hicho cha miezi mitatu kukamilisha kazi hiyo.



Utata mwingine
Wakati mvutano wa tarehe ya kura hiyo ukiendelea, imebainika kuwa wakati Hazina ikihangaika kulipa Sh149 bilioni za Mfumo wa Utambuzi wa Mpigakura wa Kielektroniki (BVR), Ofisi ya Waziri Mkuu imekataa ofa kutoka Ufaransa na Canada ya kutoa mashine 12,233 kupitia ushirikiano wa serikali kwa serikali.

Kupitia ushirikiano huo, serikali za Ufaransa na Canada zingetoa msaada katika mradi huo kwa mkopo nafuu lakini zikitaka kampuni za kusambaza mashine hizo zitoke katika moja ya nchi hizo mbili.

Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la The Citizen umeonyesha kuwa mpango huo ungegharimu Sh138.6 bilioni tofauti na Sh146.8 bilioni ambazo Tume imepanga kutumia katika mradi huo.

Kuhusu lawama za kwa nini Nec isitumie vitambulisho vya Taifa vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Jaji Lubuva alisema vitambulisho hivyo havijagawiwa katika maeneo yote nchini.

“Tutakapofika mahali, kila tunapokwenda kuna vitambulisho vya uraia, ndipo tutaweza kuvitumia wakati wa uandikishaji kwa kuwa vitatupa facts (taarifa) zote za mpigakura,” alisema.

Hata hivyo, alisema Katiba na sheria hairuhusu kazi ya uandikishaji wapigakura kufanywa na Nida... “Sheria inasema kuwa kazi ya upigaji kura itafanywa na Nec.”

Jaji Lubuva alisema vitambulisho vya Taifa vitakapoenea, mpigakura hatakuwa tena akiulizwa kitambulisho cha mpigakura, bali atatakiwa kutoa kitambulisho cha uraia.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alisema kuna mkanganyiko kati ya Mwenyekiti wa Nec na Jaji Werema kuhusu tarehe ya kufanyika kura ya maoni.

Alitaka kusahihishwa kwa kauli hizo mbili ili kuepuka mgongano kutokana na kutofautiana huko.
Hali hiyo, ilimfanya Jaji Lubuva kurudia kwa mara nyingine kusema kuwa kura ya maoni itakuwa baada ya Machi 30 mwakani.


Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, walitumia daftari ambalo lilitumika mwaka 2004, ambalo lililalamikiwa na wananchi kuwa lina kasoro nyingi hivyo uchaguzi ujao Tume yake itatumia BVR.

Jaji Lubuva alisema mfumo huo unajumuisha kamera na unamtambua mpigakura, hivyo kuondoa hofu ya mtu kuandikishwa mara mbili.

“Akija mtu ambaye ameandikishwa mahali pengine system (mtandao) inakataa. Vijana wote waliofikia kuandikishwa wataandikishwa na mfumo huu ndiyo utakaotupa uhakika zaidi,” alisema Jaji Lubuva.

Alisema mfumo huo wa BVR umetumika katika nchi nyingi za Afrika, Ghana, Liberia, Nigeria, Zambia, Afrika Kusini na Kenya na hata Zanzibar inautumia baada ya kuingia katika serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Watanzania wasione kitu cha ajabu sana, sisi tumechelewa. Halafu sisi tutatumia mfumo huu kwa kuandikisha tu na si ile wanayoita E voting (kupiga kura kwa mtandao),” alisema.

Alisema Kenya haikutumia mfumo huo katika kuandikisha pekee, bali na katika kusafirisha takwimu tofauti na Tanzania ambayo itatumia katika uandikishaji tu.
Source:Mwananchi.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top