Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid, amebainisha hayo leo Ijumaa Agosti 15, 2014 kuwa wagonjwa waliohisiwa kupata maambukizi hayo kutokana na kuwa na dalili za awali, ni wa kutoka nchini Benin na Mtanzania mmoja, na kuwa vipimo vimeonyesha kuwa hawana maambukizi hayo huku akisema vifaa maalumu vitakavyotumiwa na watoa huduma katika kuhudumia wagonjwa hao vimewekwa tayari.
Awali jana Alhamisi Agosti 14, 2014 iliripotiwa wagonjwa wawili kuhisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo jijini Dar es Salaam, hata hivyo walifikishwa katika Kituo Maalum kilichotengwa na Serikali kwa ajili ya waathirika wa wagonjwa huo kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uangalizi wa kidaktari.
Taarifa   kutoka katika Kituo hicho zimeeleza kuwa mtu mmoja Raia wa Benin anayesadikiwa kuwa na ugonjwa huo alifikishwa hospitalini hapo akitokea katika Hospitali ya MAI iliyopo jijini humo.
Gari la kubeba wagonjwa limeshuhudiwa likiingia katika Kituo hicho likitokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa waMwalimu Julius Nyerere, Julius Nyerere International Airport (JNIA), ambalo lilimfikisha mtu mmoja akitokea Uwanjani hapo huku akitokwa na damu puani huku akijiziba kwa pamba.
Akizungumzia kutengwa kwa eneo hilo, Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Grace Maghembe, amebainisha kuwa bado serikali inaendelea na maandalizi katika eneo hilo ambapo pia alithibitisha kupokelewa kwa Raia huyo wa kigeni ambapo mbali na mgonjwa huyo alisema alipelekwa mtu mwingine aliyehofiwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo katika Kituo hicho.
Katika hatua nyingine abiria wanaowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, wameanza kuchunguzwa kama wana maambukizi ya ugonjwa huo au la! 
Ofisa Afya Mfawidhi wa wa Uwanja wa Ndege, Dkt. George Ndaki, amesema kwasasa uwanja umepata vifaa ili kujikinga na ugonjwa huo wakati wa ukaguzi
Wakati haya yakitokea jijini Dar es Salaam abiria wanaoingia na kutoka nchini kupitia mpaka wa Namanga mkoani Arusha, wamezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, East African Community (EAC) kuchukua tahadhari kubwa zaidi ya kuenea kwa ugonjwa huo kwa wananchi wanaosafiri kwa njia ya barabara kutokana na hofu ya kueneza ugonjwa huo kuliko watu wanaotumia usafiri wa aina nyingine.
Wakizungumzia hatua zilizochukuliwa katika kudhibiti hali hiyo katika mpaka huo wamesema hazitoshi, ikilinganishwa na ukubwa wa tishio la ugonjwa huo hivyo wameshauri kuwepo kwa mpango wa umoja wa kudhibiti majanga kama hayo.
Baadhi ya watendaji wa Taasisi zinazotoa huduma mbalimbali katika mpaka huo, wametaka jitihada kubwa zaidi za kudhibiti ugonjwa huo kabla haujaingia katika moja ya nchi wanachama kwani itakua vigumu kuukabili ukishaingia kutokana na mwingiliano wa wananchi wan chi hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Longodo iliyopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, James Ole Milya, amesema licha ya Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya kuimarisha utendaji wake hususani wa kuhakikisha sheria za kusimamia watu wanaoingia na kutoka bado jitihada zaidi zinahitajika zikiwemo za kuelimisha wananchi.
Homa ya Ebola ilianza Guinea na kutapakaa nchi jirani za Sierra Leone na Liberia. Mashirika mawili ya ndege ya Afrika ya Arik Air la Nigeria na ASKY ya Togo yamekwisha kutangaza kuvunja safari za kwenda nchi zilizoathirika.
Dalili
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, dalili za awali za ugonjwa huo ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni.
Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, kutokwa na vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa, hutokwa damu ndani na nje ya mwili.
Katika mkoa wa Dar es Salaam, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Temeke Isolation Unit, zimetengwa maalum kwa kuhudumia wagonjwa wa ebola endapo watatambuliwa ambapo eneo la Temeke bado linaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia vigezo maalumu ili likidhi mahitaji ya matibabu ya ugonjwa huu.