Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero imeamua kufuta miliki ya mashamba yote makubwa yasiyoendelezwa na taratibu mpya zinafanyika ili kuyamilikisha kwa wananchi.
Kati ya mashamba hayo, matatu ni ya aliyekuwa
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi Balali na
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Marehemu Priva Mtema yaliyoko
katika vijiji vya Lungungole na Merera ambayo wananchi wameshayavamia na
kuendeleza shughuli za kilimo.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Kilombero juzi, Mwenyekiti wake, David Ligazio alisema
taratibu za kuomba hatimiliki za mashamba hayo zifutwe zinaendelea.
Ligazio alisema wamiliki wa mashamba hayo
wameshapewa notisi na orodha yao imeshawasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi
ili aridhie kufutwa kwa hati za mashamba hayo.
Alisema uamuzi wa kuyataifisha umekuja baada ya
halmashauri kubaini kuwa yamekuwa hayaendelezwi na hivyo kusababisha
maeneo hayo kuwa misitu wakati wananchi wanahitaji maeneo ya kulima.
Alisema ukaguzi wa kumbukumbu umeonyesha kuwa
idadi kubwa ya wamiliki hao hawapo wilayani Kilombero na maeneo hayo
yanamilikiwa kwa hati za muda mrefu bila kufuata taratibu.
Alisema utaratibu unaofanyika sasa ni kuwaagiza
watendaji na wenyeviti wa vijiji, kuanisha ukubwa halisi wa mashamba
hayo ili kurahisisha kazi ya kuyagawa kwa wananchi katika siku zijazo.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema taarifa hiyo
haijafika ofisini kwake, lakini akabainisha kuwa kuna watu wengi
wanaomiliki ardhi kubwa mkoani Morogoro bila kuwa na hatimiliki wala
kufuata taratibu huku wakiwa wanawatisha wananchi.
Aliwataka wananchi hao kujisimamia, waondoe
unyonge na kuzingatia taratibu za ardhi, kwamba inatakiwa kugawiwa
kupitia mkutano mkuu wa kijiji, vinginevyo wana haki ya kujitwalia
maeneo hayo na kufanya maendeleo mengine.
“Kuna matukio unakuta mtu anakaa na mwenyekiti wa
kijiji na kujifungia, wanajadili wenyewe na kugawiana maeneo ya kijiji
bila kuwashirikisha wananchi, hawa wananchi wanatakiwa kukataa hali
hiyo,” alisema.
Maeneo yanayogawiwa
Mwenyekiti wa halmashauri aliyataja maeneo
mashamba yanayotakiwa kugawanywa kwa wananchi na ukubwa wake katika
mabano kuwa ni Lungongole (ekari 375) na Merea (ekari 373). Pia kuna
shamba lenye ukubwa wa hekta 887 linalomilikiwa na Balali, ekari 491
zinazomilikiwa na George Teni katika Kijiji cha Kisegese na ekari 500
zinazomilikiwa na Aloyce Lyenga katika Kijiji cha Idete.
Katika orodha hiyo pia kuna ekari 30,000 za Kampuni ya Merera Plantation Ltd katika Kijiji cha Merera.
Mashamba mengine ni ekari 102 za Abdallah Sajiri
zilizopo Kining’ina, ekari 295 za Peter Warwic zilizopo Lumemo, ekari
484.9 za Sadru Meghji zilizopo Msolwa Ujamaa, ekari 120 za Ranifa EC
&DEV. Group zilizopo Kisegese na hekta 5,128 za Rubada zilizopo
Ngalimila.
Ligazio alitaja mashamba mengine kuwa ni ekari
2,390 za kampuni iliyokuwa ya usafirishaji mkoani Morogoro zilizopo
Mbingu, ekari 875 za Jerome Mwakifuna zilizopo Idete, ekari 656 za Priva
Mtemanyanja zilizopo Lungongole na ekari 1,500 za Ngwasi River Valley
Inv. zilizopo Mlimba
Post a Comment