Mawaziri watano wa Serikali inayomaliza muda wake wameanguka kwenye
uchaguzi majimboni mwao, sambamba na wagombea wengine maarufu wa Bunge
lililopita baada ya matokeo ya kura zilizopigwa Jumapili kuanza
kutangazwa jana.
Mawaziri hao wanaungana na wabunge wengine maarufu wa Bunge la Kumi
walioshindwa kutetea majimbo yao, wakiwamo wa kambi ya upinzani ambao
wameangushwa na wagombea wa CCM.
Pia wamo mawaziri wa zamani wawili, Cyril Chami na Omary Nundu
walioanguka kwenye uchaguzi, kwa mujibu wa matokeo ambayo yanaendelea
kutangazwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema jana kuwa itakamilisha kazi ya kutangaza matokeo yote keshokutwa.
Mawaziri walioanguka kwenye uchaguzi huo ni Steven Wasira,Christopher Chiza, Aggrey Mwanri, Dk Steven Kebwe na Anne Kilango.
Katika matokeo yaliyotangazwa jana, Wasira, kada maarufu na mwanasiasa
mkongwe aliyekuwa akitetea Jimbo la Bunda, alijikuta akiangushwa na
mwanasiasa kijana, Ester Bulaya, ambaye alihamia Chadema baada ya Bunge
la Kumi kumaliza muda wake.
Wasira, ambaye alikuwa Waziri wa Kilimo na Chakula, alianza mchakato wa
uchaguzi mwaka huu kwa kuomba ridhaa ya CCM agombea urais, lakini
hakupitishwa. Bulaya, ambaye alikuwa mbunge wa viti maalum (CCM),
alipata kura 28, 508 na kumuacha mbali waziri huyo mkongwe aliyepata
kura 19, 126.
Mwingine aliyeanguka ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwezeshaji
na Uwekezaji, Christopher Chiza ambaye ameangushwa na Bilago Samson wa
Chadema katika Jimbo la Buyungu. Waziri huyo alizidiwa kwa kura 104
baada ya Samson kupata kura 23,041 dhidi ya 22,934 za Chiza.
Lakini hali haikuwa hivyo kwa Naibu Waziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri
kwenye Jimbo la Siha. Waziri huyo alizidiwa kwa zaidi ya kura 4,100 na
mpinzani wake kutoka Chadema, Dk Godwin Mollel aliyepata kura 22,746.
Katika Jimbo la Serengeti, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Stephen Kebwe pia alijikuta akipoteza nafasi ya kurudi bungeni kwa kura
alipoangushwa na Marwa Ryoba wa Chadema. Dk Kebwe alipata kura 39,232,
akiwa amezidiwa na mpinzani wake kwa zaidi ya kura 820.
Anne Kilango, ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu mwaka 2013
baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyosababishwa na kashfa ya
Operesheni Tokomeza, ameangushwa na mgombea wa Chadema, Naghenjwa
Kaboyoko wa Chadema kwa tofauti ya kura 3,297.
Kilango alipata kura 15,539 wakati mgombea huyo wa Chadema alipata kura
18,836. Pia wabunge maarufu kama Vincent Nyerere (Musoma Mjini), James
Lembeli (Kahama Mjini) na Kyisieri Chambiri (Babati Mjini) wameangushwa.
Nyerere, aliyekuwa akitetea kiti cha Musoma Mjini kwa tiketi ya Chadema,
aliachwa mbali na mgombea wa CCM, Vedastus Mathayo aliyepata kura 32,
836 dhidi ya 25,549.43 za Nyerere.
Lembeli, ambaye alihamia Chadema muda mfupi baada ya Bunge la Kumi
kumaliza muda wake, aliachwa mbali na mfanyabiashara maarufu, Jumanne
Kishimba aliyepata kura 47,553 dhidi ya kura 30,122 za Lembeli.
Post a Comment