Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amemhakikishia Waziri Mkuu wa Israel kuwa Serikali ya awamu ya
tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kushirikiana na
kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na Israel katika nyanja
mbalimbali ili kuleta manufaa kwa pande zote.
Rais Magufuli amesema hayo alipokutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa Israel hapa nchini mwenye makazi yake Mjini
Nairobi - Kenya Mheshimiwa Yahel Vilan, Ikulu Jijini Dar es salaam.
"Natambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na
Israel, mahusiano haya ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi zetu mbili,
nataka mahusiano haya yaimarishwe zaidi " Alisema Dkt. Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameahidi kuwa Tanzania itahakikisha inaanzisha ubalozi wake nchini Israel haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake Balozi wa Israel hapa nchini Mheshimiwa
Yahel Vilan pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri
iliyofanywa na uongozi wake katika kipindi kifupi cha miezi miwili tangu
aingie madarakani amemhakikishia kuwa Israel itaendelea kushirikiana na
Tanzania na ipo tayari kuimarisha zaidi mahusiano.
Balozi Vilan ametaja baadhi ya maeneo ya ushirikiano katika
uchumi kuwa ni pamoja na Kilimo, Maji, Ufugaji wa Nyuki na Sayansi na
Teknolojia huku akibainisha kuwa Israel imewaalika Jumuiya ya
wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika Kongamano la biashara kati
ya Tanzania na Israel litakalofanyika Mjini Tel Aviv nchini Israel,
mwezi Septemba mwaka huu.
Balozi Vilan pia ameahidi kufikisha ujumbe wa Rais Magufuli
kwa Waziri Mkuu wa Israel Mheshimiwa Benjamin Netanyahu na pia ameahidi
kuanzisha ofisi ya kutoa huduma ya visa hapa nchini haraka
iwezekanavyo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam.
19 Januari, 2016
Post a Comment